“Katika mazingira ya sasa yenye changamoto nyingi za mabadiliko ya kijamii, kiuchumi, kiteknolojia na athari za utandawazi, ni dhahiri kuwa malezi bora ya watoto wetu ndiyo silaha muhimu ya kuimarisha maadili, uzalendo, na uwajibikaji katika kizazi cha sasa na kijacho kwa lengo la kuleta matokeo chanya kwa Taifa letu”.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Kenani Kihongosi akifungua kongamano la wazazi kuhusu malezi bora kwa ustawi wa jamii na maendeleo endelevu ya Taifa la leo na kesho.
Kongamano hilo limefanyika mkoani Simiyu likiwa na malengo mahususi ambayo ni:
- Kuwajengea wazazi maarifa na mbinu za kisasa za malezi bora.
- Kuimarisha nafasi ya mzazi kama kiongozi wa familia na mlezi wa kwanza wa mtoto.
- Kuelimisha jamii juu ya mbinu za mawasiliano na msaada wa kijamii ndani ya familia.
Kusaidia juhudi za Serikali katika kukuza maadili, nidhamu, na mshikamano wa kitaifa.
Image
Mkuu huyo wa mkoa amshukuru Mkurugenzi wa Taasisi ya Soul & Mind Youth Counselling Bi. Adelina Ikonje na Timu yake kwa kuandaa kongamano hilo muhimu sana linalolenga kuhamasisha na kujenga uelewa wa wazazi kuhusu umuhimu wa malezi bora kwa ustawi wa familia, Jamii na maendeleo endelevu ya taifa letu kwa ujumla.
Pia ameahidi kuwa Serikali ya Mkoa wa Simiyu itaendelea kushirikiana na wadau wote ili kuhakikisha kuwa juhudi hizi zinafanikiwa kwa kiwango cha juu.
Ni ukweli usiopingika kuwa familia imara hujengwa na wazazi wenye maarifa sahihi, mfano bora, na mawasiliano chanya katika kulea watoto wao ambao ndio taifa la kesho na endelevu.
